Nomino huwakilishwa na herufi (N).

Ni aina za maneno ambazo zinataja jina la mtu, mahali, vitu.

Kwa mfano:

Juma, shule, Nairobi n.k.

Kuna aina sita za Nomino za Kiswahili:

  • Nomino za Kawaida
  • Nomino za Kipekee
  • Nomino za Jamii/Makundi
  • Nomino za Kitenzi-Jina
  • Nomino za Dhahania
  • Nomino za Wingi

Nomino za Kawaida

Haya ni majina ya kawaida, na yanataja majina ya vihusika kwa jumla.

Kwa mfano,neno “watu” ni jina la kawaida, halitaji jina la mtu maalum.

Mifano mingine ni pamoja na: walimu/mwalimu, miji/mji, mito n.k.

Nomino za Kipekee

Ni majina maalum yanayotaja mtu, kitu, mahali n.k. Kwa mfano: Musa, Kisumu, Ziwa Viktoria.

Nomino zote za Kipekee huandikwa kwa kuanza na herufi kubwa.

Kwa mfano, sio sahihi kuandika nomino Musa kama musa.

Nomino za Makundi/Jamii

Nomino hizi hutumiwa kutaja kundi la vitu, watu, wanyama n.k.

Kwa mfano; umati wa watu, mkungu wa ndizi, bumba la majani n.k.

Nomino za Vitenzi –Jina

Nomino hizi huundwa kwa kuongeza “KU” kwenye vitenzi kama kiambishi awali.

Kwa mfano, kwenye nomino “Kucheza”:

Ku (kiambishi awali) + cheza(kitenzi).

Mifano mingine ni kama vile kufa, kula, kuja.

Nomino hizi hupatikana katika ngeli ya KU-KU; mfano kwenye sentesi: Kuja kwake kulinijaza furaha tele.

Nomino za Dhahania

Nomino za Dhahania ni majina ya vitu ambavyo haviwezi kuguswa, kuonekana; tunaweza tu kuzihisi kupitia hisia.

Kwa mfano, neno Upendo ni nomino dhahania kwa sababu hatuwezi kushika wala kuona upendo; upendo ni hisia.

Yaani nomino hizi zipo tu kwenye dhahana zetu.

Mifano: njaa, baridi, malaika (viumbe vya kidhahania ambavyo vinapatikana kwenye Biblia), uchovu n.k.

Nomino za Wingi

Nomino hizi hurejelea vitu vyote ambavyo haviwezi kuhesabiwa

kwa mfano, sukari, mafuta, maji, mchanga, chumvi n.k.