Vivumishi huwakilishwa na herufi (V).

Ni aina za maneno ambazo hutoa maelezo zaidi kuhusu nomino; mfano katika sentensi: Mwanafunzi (N) hodari (V); kwenye mfano huu, neon “hodari” linaelezea zaidi kuhusu mwanafunzi ambayo ni nomino.

Kwa kawaida, vivumishi hutanguliwa na nomino.

Kuna aina tisa za Vivumishi:

  • Vivumishi vya Sifa
  • Vivumishi vya Idadi
  • Vivumishi Viashiria
  • Vivumishi Vimilikishi
  • Vivumishi Visisitizi
  • Vivumishi Viulizi
  • Vivumishi Virejeshi
  • Vivumishi Vya A-Unganifu
  • Vivumishi Vya KI-Mfanano

Vivumishi Vya Sifa

Hizi ni aina za vivumishi ambazo hueleza sifa ya nomino katika sentensi.

Kwa mfano:

  • Mtoto mtiifu amepita mtihani
  • Gari kubwa liliendeshwa kwa kasi.

Vivumishi Vya Idadi

Aina hii ya vivumishi hutoa taarifa kuhusu idadi ya nomino au kiwakilishi cha nomino.

Idadi inaweza kuwa kamili/halisi au jumla.

Kwa mfano:

  • Wanafunzi wawili walifukuzwa shuleni (Wawili inaonyesha idadi halisi ya wanafunzi).
  • Wanafunzi wachache walifukuzwa shuleni (wachache ni idadi kwa jumla).

Vivumishi Viashiria

Pia vinajulikana kama vivumishi vionyeshi.

Vinatumiwa kuonyesha umbali wa nomino kutoka kwa mzungumzaji; na ni aina tatu: vya karibu, vya mbali kidogo na vya mbali sana. Mifano, hii, hiyo, ile; hapa, hapo, pale.

Mifano katika sentensi:

  • Gari hili lilinunuliwa jana.
  • Gari hilo liliendeshwa kwa kasi.
  • Gari lile liliibwa juzi.

Vivumishi Vimilikishi

Hutumika kuonyesha nomino inayomiliki nyingine; na mizizi yake huundwa kwa: -angu, -ake, -ako, -etu, -ao n.k.

Mifano katika sentensi:

  • Mtoto wake alipotea.
  • Vitabu vyao vilipendeza.

Vivumishi Visisitizi

Aina hizi za vivumishi vinatumika kusisitiza nomino.

Huundwa kutokana na vivumishi vionyeshi, kisha kuvirudiarudia.

Kwa mfano:

  • Mtoto yuyu huyu
  • Kitabu kiki hiki
  • Mahali papo hapo n.k.

Vivumishi Viulizi

Hutumika kuuliza swali.

Baadhi huchukua viambishi vya ngeli kama vile: -ngapi?; -pi?; gani?

Mifano katika sentensi:

  • Watu gani walitumwa mjini?
  • Vitabu vingapi vilipotea?
  • Gari lipi liliharibika?

Vivumishi Virejeshi

Hurejelea nomino iliyotajwa au kiwakilishi cha nomino.

Kuna aina mbili za vivumishi virejeshi: amba- rejeshi na -o rejeshi.

Mifano katika sentensi:

  • Watoto ambao walipotea juzi wamepatikana (amba- rejeshi)
  • Watoto waliopotea juzi wamepatikana (-o rejeshi).

Vivumishi Vya A-Unganifu

Huonyesha uhusiano baina ya nomino mbili, na hutumia mzizi wa –a unganifu.

A-unganifu huchukua ngeli ya nomino husika.

Kwa mfano:

  • Kitabu cha mwanafunzi kiliraruka
  • Mtoto wa mama alianguka
  • Tunda la babu lilioza.

Vivumishi Vya KI ya Mfanano

Hutumiwa kuonyesha mfanano wa sifa ya nomino na hali/tabia nyingine.

Hutumia kiambishi awali –ki-. Mifano:

  • Mavazi ya kiume
  • Vyakula vya kijeshi.