Ngeli ni vikundi vya nomino ya Kiswahili.

Ngeli hizi hutokana na viambishi ambavyo nomino huchukua katika hali ya umoja na wingi.

Ngeli husaidia katika upatanisho wa kisarufi. Zifuatazo ndizo ngeli za Kiswahili:

A-WA

Ngeli hii huhusisha majina ya viumbe vyote vyenye uhai isipokuwa mimea. Ngeli hii huchukua kiambishi ‘a’ kwa umoja na “wa’ kwa wingi katika upatanishaji wa kisarufi. Kwa mfano:

Mtoto alienda (umoja)

Watoto walienda (wingi)

U-I

Nomino za ngeli hii huanza na “m” kwa umoja na “mi” kwa wingi na huchukua kiambishi cha upatanisho wa kisarufi ‘u’ kwa umoja na ‘i’ kwa wingi. Kwa mfano:

a. Mti utakatwa (umoja) b. Miti itakatwa (wingi)

Mifano zaidi: mkate-mikate, mlango-milango, mwiko-miiko, mkoba-mikoba

U-YA

Majina haya huchukua kiambishi ‘u’ kwa umoja na ‘ya’ kwa wingi kwenye upatanisho wa kisarufi. Aidha, nomino hizi huanza na ‘u’ kwa umoja na ‘ma’ kwa wingi. Kwa mifano:

1. Ugonjwa ulienea (umoja) - Magonjwa yalienea (wingi)

Mifano zaidi: ulezi-malezi, uuaji-mauaji n.k.

YA-YA

Majina haya huchukua kiambishi ‘ya’ kwa umoja na kwa wingi kwenye upatanisho wa kisarufi. Vile vile, majina haya huanza na kiambishi ‘ma’ kwa umoja na kwa wingi. Aidha, nomino hizi huwa haziwezi kuhesabika. Kwa mfano:

Maji yalimwagikwa (umoja)- Maji yalimwagika (wingi)

Mafuta yalichafuka- Mafuta yalichafuka

Maziwa yalikuwa matamu- Maziwa yalikuwa matamu

LI-YA

Majina haya huwa hayana kiambishi maalum kwa umoja lakini huchukua kiambishi ‘ma’ kwa wingi kwenye upatanisho wa kisarufi. Aidha, nomino zote katika hali ya ukubwa hupatikana kwenye ngeli hii. Kwa mfano:

Gari liliendeshwa kwa kasi (umoja) - Magari yaliendeshwa kwa kasi (wingi)

Jitu liliwashtua wanakijiji (ukubwa/umoja) – Majitu yaliwashtua wanakijiji (Ukubwa/wingi)

Mifano zaidi: tunda/matunda, jino/meno,

KI-VI

Nomino zenye sifa zifuatazo hupatikana katika ngeli hii; (1) majina yanayoanza na silabi ‘ch’ kwa umoja na silabi ‘vy’ kwa wingi. (2) nomino ambazo hutangulia kwa silabi ‘ki’ kwa umoja na ‘vi’ kwa wingi. (3) nomino zote katika hali ya udogo hupatikana katika ngeli.

Nomino hizi huchukua kiambishi ‘ki’ kwa umoja na ‘vi’ kwa wingi kwenye upatanisho wa kisarufi. Kwa mfano:

a. Kiti kilivunjika- Viti vilivunjika

b. Chumba kilisafishwa- Vyumba vilisafishwa

c. Kitoto kilichapwa na mwalimu- Vitoto vilichapwa na walimu

I-ZI

Majina haya huchukua kiambishi ‘i’ kwa umoja na ‘zi’ kwa wingi kwenye upatanisho wa kisarufi. Baadhi ya majina haya huanza na n, na huwa hayabadiliki kwa wingi. Kwa mfano:

a. Nyumba ilibomolewa- Nyumba zilibomolewa

b. Nguo ilioshwa- Nguo zilioshwa

Mifano zaidi: nchi, nyundo, ngoma n.k.

I-I

Majina haya huchua viambishi vya upatanisho wa kisarufi ‘i’ katika umoja na wingi. Kwa mfano:

a. Sukari ilimwagika- Sukari ilimwagika

b. Njaa ilizidi- Njaa ilizidi

U-ZI

Nomino hizi huchukua viambishi vya upatanisho wa kisarufi ‘u’ katika umoja na ‘zi’ katika wingi. Baadhi ya nomino hizi huanza na u katika umoja na n katika wingi. Kwa mfano:

a. Uzi ulipotea- Nyuzi zilipotea

b. Ufa ulizibwa- Nyufa zilizibwa

c. Wimbo ulipendeza- Nyimbo zilipendeza

U-U

Majina katika ngeli hii huwa ni ya vitu visivyowezakuhesabika wala haviwezi kugawanyika. Aidha, baadhi ya nomino dhahania hutokea kwenye ngeli hii.

Nomino hizi huchukua kiambishi cha upatanisho wa kisarufi ‘u’ katika umoja na wingi. Kwa mfano:

a. Unga ulimwagika wote- Unga ulimwagika wote

b. Upendo ulienea kote- Upendo ulienea kote.

Mifano zaidi: Uji, ugali, ugoro n.k.

KU

Ngeli hii huhusisha nomino zote za kitenzi-jina; na huchukua kiambishi cha upatanisho wa kisarufi ‘ku’ katika umoja na wingi. Kwa mfano:

a. Kusoma kwangu kulinisaidia- Kusoma kwetu kulitusaidia.

b. Kulala kwako kunaudhi- Kulala kwenu kunaudhi.

PA-KU-MU

Hii ni ngeli ya mahali.

  • PA (Mahali karibu au panapodhihirika) kwa mfano: kiti kipo pale
  • KU (Mahali mbali au kusikodhihirika) kwa mfano: Mahali kule kunafaa
  • MU (ndani ya) kwa mfan: Nyumbani mle mna fujo.