Vivumishi huwakilishwa na herufi (V).
Ni aina za maneno ambazo hutoa maelezo zaidi kuhusu nomino; mfano katika sentensi: Mwanafunzi (N) hodari (V); kwenye mfano huu, neon “hodari” linaelezea zaidi kuhusu mwanafunzi ambayo ni nomino.
Kwa kawaida, vivumishi hutanguliwa na nomino.
Kuna aina tisa za Vivumishi:
- Vivumishi vya Sifa
- Vivumishi vya Idadi
- Vivumishi Viashiria
- Vivumishi Vimilikishi
- Vivumishi Visisitizi
- Vivumishi Viulizi
- Vivumishi Virejeshi
- Vivumishi Vya A-Unganifu
- Vivumishi Vya KI-Mfanano
Vivumishi Vya Sifa
Hizi ni aina za vivumishi ambazo hueleza sifa ya nomino katika sentensi.
Kwa mfano:
- Mtoto mtiifu amepita mtihani
- Gari kubwa liliendeshwa kwa kasi.
Vivumishi Vya Idadi
Aina hii ya vivumishi hutoa taarifa kuhusu idadi ya nomino au kiwakilishi cha nomino.
Idadi inaweza kuwa kamili/halisi au jumla.
Kwa mfano:
- Wanafunzi wawili walifukuzwa shuleni (Wawili inaonyesha idadi halisi ya wanafunzi).
- Wanafunzi wachache walifukuzwa shuleni (wachache ni idadi kwa jumla).
Vivumishi Viashiria
Pia vinajulikana kama vivumishi vionyeshi.
Vinatumiwa kuonyesha umbali wa nomino kutoka kwa mzungumzaji; na ni aina tatu: vya karibu, vya mbali kidogo na vya mbali sana. Mifano, hii, hiyo, ile; hapa, hapo, pale.
Mifano katika sentensi:
- Gari hili lilinunuliwa jana.
- Gari hilo liliendeshwa kwa kasi.
- Gari lile liliibwa juzi.
Vivumishi Vimilikishi
Hutumika kuonyesha nomino inayomiliki nyingine; na mizizi yake huundwa kwa: -angu, -ake, -ako, -etu, -ao n.k.
Mifano katika sentensi:
- Mtoto wake alipotea.
- Vitabu vyao vilipendeza.
Vivumishi Visisitizi
Aina hizi za vivumishi vinatumika kusisitiza nomino.
Huundwa kutokana na vivumishi vionyeshi, kisha kuvirudiarudia.
Kwa mfano:
- Mtoto yuyu huyu
- Kitabu kiki hiki
- Mahali papo hapo n.k.
Vivumishi Viulizi
Hutumika kuuliza swali.
Baadhi huchukua viambishi vya ngeli kama vile: -ngapi?; -pi?; gani?
Mifano katika sentensi:
- Watu gani walitumwa mjini?
- Vitabu vingapi vilipotea?
- Gari lipi liliharibika?
Vivumishi Virejeshi
Hurejelea nomino iliyotajwa au kiwakilishi cha nomino.
Kuna aina mbili za vivumishi virejeshi: amba- rejeshi na -o rejeshi.
Mifano katika sentensi:
- Watoto ambao walipotea juzi wamepatikana (amba- rejeshi)
- Watoto waliopotea juzi wamepatikana (-o rejeshi).
Vivumishi Vya A-Unganifu
Huonyesha uhusiano baina ya nomino mbili, na hutumia mzizi wa –a unganifu.
A-unganifu huchukua ngeli ya nomino husika.
Kwa mfano:
- Kitabu cha mwanafunzi kiliraruka
- Mtoto wa mama alianguka
- Tunda la babu lilioza.
Vivumishi Vya KI ya Mfanano
Hutumiwa kuonyesha mfanano wa sifa ya nomino na hali/tabia nyingine.
Hutumia kiambishi awali –ki-. Mifano:
- Mavazi ya kiume
- Vyakula vya kijeshi.