Viwakilishi huwakilishwa na herufi W.
Ni aina za maneno ambazo hutumiwa kuwakilisha nomino; yaani viwakilisha hutumiwa badala ya nomino.
Kwa mfano, badala ya kusema: Yeye ni mtoto mtiifu. Yeye inawakilisha nomino katika sentensi hii.
Kuna aina nyingi za viwakilishi vya Kiswahili:
Viwakilishi vya Nafsi
Hutumika badala ya nomino zinazotaja nafsi; vinaweza kutokea kwa umoja au wingi.
Kwa mfano: Mimi- Sisi; Wewe-Nyinyi; Yeye- Wao
Viwakilishi Vionyeshi
Kwa mfano:
- Hawa wanasumbua.
- Wale wataimbia wageni.
Viwakilishi Viulizi
Kwa mfano:
- Yupi ataimbia wageni?
- Lipi lilioza?
Viwakilishi Vimilikishi
Kwa mfano: Lake lilipotea (Lake linaeza kuwa linawakilisha kitu chochote kinachopatikana katika ngeli ya LI-YA kama vile; tunda, gari).
Viwakilishi Virejeshi
Vinarejelea nomino; kama vile: Ambacho kilipotea; Kilichopotea; Ambaye alipotea; Aliyepotea.
Viwakilishi vya Sifa
Kwa mfano: Wazuri watatuzwa; Warefu wataajiriwa; Watiifu walitumiwa kama mfano.
Viwakilishi vya Idadi
Kama vile: Wawili walitumwa; Saba watasafiri kesho.
Idadi hizi za Kiswahili huwa hazichukui viambishi ngeli- sita, saba, tisa, kumi. Kwa hivyo, ni makosa kusema: wasita, wasaba, watisa, wakumi.
Viwakilishi vya Pekee
Hubainisha nomino inayotajwa.
Huchukua muundo wa –ote, o-ote, -enye, -enyewe na ingine.
Kwa mfano:
- Yeyote atatumwa (ngeli za A-WA huwa yeyote kwa umoja).
- Chochote kitatumika.
- Mwenyewe atafua.
- Mwenye gari atatumwa.
- Kingine kilitupwa.
Viwakilishi vya A-Unganifu
Ni kama vile tu vivumishi vya sifa ila tu nomino hazitajwi kwenye viwakilishi.
Kwa mfano; Cha mama kilipotea; Ya wazee yaliibwa.